Ziko wapi ahadi tulizopewa na serikali ya Jubilee?

Ni takriban miaka saba sasa tangu serikali ya Rais Uhuru Kenyatta kuchukua hatamu. Walipojipigia debe, walituahidi mambo mengi na kutufanya kuwapa kura. Lakini je, miaka michache kabla hatamu yao kuisha, ahadi zimetimizwa?

Utafiti unaonyesha kuwa kwa miaka mitatu sasa, gharama ya maisha imekua ikipanda kwa viwango vikubwa. Mafuta yanaagizwa kutoka mataifa ya nje yakiuzwa nchini kwa bei ghali. Kwa nini tununue mafuta kwa bei ghali na tuna mafuta ya kutosha hapa nchini?

Tulipewa ahadi ya viwanja vya michezo, ambavyo vingekuwa kwa viwango vya kimataifa. Hadi sasa, bado wachezaji wa vilabu vya humu nchini wanalazimika kusafiri mwendo mrefu ili kupata viwanja vya kucheza. Tutakuzaje vipaji iwapo vijana wetu hawana viwanja vya kuchezea? Serikali iliahidi kuinua viwango vya michezo nchini lakini sasa ligi kuu nchini inakaribia kuanguka. Serikali iko wapi ligi kuu nchini inapoyumbayumba.

Ajira ni mojawapo ya ahadi ambazo mpaka leo hazijatimizwa. Visa vya wizi na ugaidi vimezidi nchini kwani vijana hawana ajira ya kuwapa mapato ili kujikimu kimaisha. Ushuru umepandishwa na serikali kuu na kusababisha kampuni nyingi kuwasimamisha kazi wafanyakazi wao, kutokana na ukosefu wa hela za kuwalipa.

Ni kinaya kuona kuwa watu tuliowachagua kutupa maendeleo, ndio wanatuibia. Je, ni magavana wangapi wameshikwa kwa kufuja mali ya umma? Ikumbukwe kuwa sisi ndio tuliwapa kura ili watuwakilishe kama viongozi wetu. Ila, tunazidi kutatizika kwani baadhi yao wanajinufaisha, kabla ya kutushughulikia sisi tuliowaamini na masuala yetu.

Sio kwamba viongozi wote ni wabaya, ila wengi wao ni wabaya, wezi na fisadi. Kabla ya serikali kumaliza hatamu yake, ihakikishe kuwa imetimiza ahadi zake kwa wananchi. Wahakikishe pia wamekabiliana na janga la ufisadi, ili pesa zinazoibiwa na viongozi walafi, zirudishwe kwa mikono ya wananchi na kuwapa maendeleo. Wananchi pia tujiangalie. Mwaka wa kura utakapowadia tuwachague viongozi watakaotufaa kimaendeleao.

PIA SOMA: Hazina ya kitaifa kuzuia fedha kwa kaunti kumi na tano