Wanyama pori watakuwa kero hadi lini?

Mola katuumba binadamu pamoja na wanyama. Kati ya wanyama, kuna wale tunaowafuga na kuna wale wanaoishi porini. Wanyama pori hawafugwi, kwani ni tishio kwa maisha ya binadamu. Kutokana na hili, ndio sababu ya kuundwa bodi ya wanyama pori ya KWS, ambayo huwatunza wanyama hawa. Lakini je, bodi hii imeshindwa na kazi?

Ni kama KWS wameshindwa na kazi. Ongezeka la visa vya wanyawa pori, kuwasumbua wananchi nyumbani kwao si mara ya kwanza jambo hili kutokea.

Hivi majuzi, simba wamewasumbua wakazi wa kaunti ya Samburu, baada ya kutoroka mbugani. Wakazi wa kule wamelazimika kutembea kwa vikundi, na kuepuka safari za usiku, ili kuepuka makali ya mnyama huyu hatari. Maafisa wa KWS wako wapi kuingilia kati na kuwaondolea wananchi kero hili?

Mbali na mifugo wa nyumbani kuliwa na wanyama hawa, mimea pia huharibiwa. Wanyama kama vile ndovu wanapoingia katika makazi ya watu husababisha uharibifu wa mamilioni ya pesa. Kinachositikisha zaidi ni jinsi serikali imekosa serikali kuwajibika, na kuwafidia wanaoathirika na kuwaacha waathiriwa wakiteseka.

Kutokana na nyongeza ya visa hivi, ni dhahiri kuwa suluhisho linafaa kutafutwa. Itakuwa vyema iwapo serikali itawekeza zaidi katika bodi ya KWS, kupitia njia zifuatazo:

1. Askari wanaoshughulika na wanyama pori kupewa mafunzo ya hali ya juu kuhusu jinsi ya kukabili kero hili.

2. Askari wavivu na wasiowajibika kikazi kuachishwa kazi. Ni jambo la kukeketa maini kuona jinsi maafisa hawa hulaza damu, wakati wanyama hawa wanawasumbua wananchi.

Iwapo serikali haitashughulika, basi wananchi wasilaumiwe kwa kuchukua sheria mikononi na kuwaua wanyama hawa. Ijapokuwa tunawahitaji kwa utalii kuendelea nchini, maisha ya wananchi wetu ni muhimu zaidi.

PIA SOMA: Ziko wapi ahadi tulizopewa na serikali ya Jubilee?