Wanafunzi 30,000 wakosa nafasi katika shule za sekondari walizochagua

Katibu mkuu wa mafunzo ya kiufundi Kevit Desai,Katibu mkuu wa wizara ya elimu Dt. Belio Kipsang, Katibu mkuu wa elimu ya juu Colleta Suda na Waziri wa elimu George Magoha wakizindua matokeo ya uteuzi wa wanafunzi katka sekondari Disemba 2, 2019.

Mwanafunzi aliyefanya vizuri zaidi katika mtihani wa cheti cha kuhitimu shule ya msingi KCPE Andy Munyir atajiunga na shule ya upili ya Alliance. Alipata alama 440 kwa 500.

Wanafunzi wa kike walioshikilia nafasi ya pili vilevile, June Jeptoo na Onyango Flavian waliojizolea alama 439 kila mmoja, walipata nafasi katika shule za wasichana za Pangani na Alliance mtawalia.

Kwa watahiniwa 1,083,456 waliofanya mtihani huo 1,075,201 wamepata nafasi katika shule za upili.

Wanafunzi 33,099 watajiunga na shule za kitaifa huku 184,816 wakijiunga na shule za mikoa, 188,454 watajiunga na shule za kaunti huku waliosalia 669,145 wakipata nafasi katika shule za kaunti ndogo.

“Wanafunzi 777 wenye ulemavu wamepata nafasi katika shule za walemavu walizochagua. Kwa jumla wanafunzi 1,246 wamepata nafasi katika shule za aina mbalimbali,” Magoha alisema.

Aidha, waziri Magoha alisema wanafunzi 30,000 watakosa kujiunga na shule walizochagua kutokana na upungufu wa nafasi katika shule hizo.

“Mwaka huu, tuligundua kuwa watahiniwa waliokuwa na uwezo wa kuzoa alama za juu katika mtihani wa KCPE walichagua shule chache. Imetokea kwamba shule hizi tajika ambazo wanafunzi wengi hutazamia kujianga nazo hazina nafasi za kutosha.” Magoha alisema.

Wanafunzi kutoka sehemu za mashinani watanufaika zaidi kwani wengine walipata nafasi katika shule za kitaifa licha kupata alama chini ya mia nne. Waziri Magoha aidha alionya walimu wakuu kuzuia wanafunzi kujiunga na shule kutokana na ukosefu wa karo.

Magoha aliongeza kuwa wanafunzi hao wataanza kujiunga na shule zao mpya kuanzia tarehe kumi na tatu Januari huku tarehe ya mwisho ikiwa Januari kumi na saba.

Kusoma habari zetu katika lugha ya Kiingereza bonyeza hapa.