Vifo Barabarani

Kwa mujibu wa takwimu zilizotolewa mwezi wa Oktoba mwaka huu na halmashauri inayodhibiti usafiri wa umma NTSA, mwaka huu kumekua na nyongeza katika ajali za barabarani, kwa takriban ajali 800 zaidi ikilinganishwa na mwaka uliopita .

Je, nani wa kulaumiwa kwa nyongeza ya ajali hizi?

Ni jambo la kushangaza kuona polisi wa trafiki walivyojaa barabarani na bado ajali zinakithiri. Je, kazi ya polisi hawa ni nini? Ripoti ya EACC yaonyesha kuwa idara ya polisi ni moja ya idara fisadi mno nchini. Twaelekea wapi kama nchi?

Habari ambazo zinachipuka kutoka kwa idara ya polisi zaashiria kuwa huenda vifaa vya Alco-blow vikatolewa barabarani kutokana na kukithiri kwa ufisadi, kwani polisi wameonekana wakiwaachia madereva walevi baada ya kupokea hongo. Je, ikiwa walinda usalama ndio wanaoendeleza ufisadi, tutawahi kustawi kama nchi?

Haya ni maswali ya ya Wanjiku aliyempoteza jamaa wake kwa ajali ya barabarani. Maswali haya yanaulizwa na mwananchi aliye na uchungu, baada ya kufanywa kilema, kutokana na ajali hizi.

Tusipoziba ufa, tutajenga ukuta kwa kupotea maisha zaidi katika ajali. Kulingana na NTSA, idadi kubwa ya waliofariki ni wanaotembea barabarani. Je, kwa nini raia asiye na hatia afe kutokana na uzembe wa mwendeshaji gari au pikipiki?

Sheria za barabarani zifuatwe na watumizi wote wa barabara na wanaokiuka sheria wakamatwe na kuadhibiwa vikali.

Madereva na polisi wanaotilia maanani kazi yao watuzwe vilivyo ili kuwapa motisha wengine kufuata mtindo huo.

Nina imani kuwa iwapo sote tutasimama pamoja, tutaliangamiza na kulipiga teke janga hili la ajali nje ya taifa letu.

Kusoma habari zetu katika lugha ya Kiingereza bonyeza hapa.