Twaelekea wapi Wakenya?

TwaelekeaWanafunzi wa Shule ya Upili ya Itiero, Kisii wakijaribu kunusuru vichache walivyobakishiwa na moto.

Twaelekea wapi? Hili ni swali ambalo Wakenya wengi wanaendelea kujiuliza kutokana na misururu ya visa vya utovu wa nidhamu ambavyo vimeshuhudiwa katika shule nyingi za upili hapa nchini.

Mali ya mamilioni ya pesa yameteketea baada ya wanafunzi wa shule nyingi za malazi za wavulana na wasichana kutekeleza uhalifu huo. Ni jambo la kusikitisha kuona wanafunzi wengi wao wenye umri wa kati ya miaka kumi na mitano na kumi na minane wakijihusisha katika visa vya uhalifu. Katika baadhi ya shule tajika, walimu kadhaa walijipata matatani wakati wanafunzi walipozua kivangaito na wakajeruhiwa. Mwanafunzi kumpiga mwalimu wake na kumjeruhi! Ajabu, tena ajabu kubwa. Chambilecho ukistaajabu ya chawa utayaona ya kunguni.

Katika miaka ya hivi karibuni visa hivi vimekuwa vingi huku vikiacha hasara kubwa ya mali, kupoteza wakati, baadhi wa wanafunzi kuathirika kisaikolojia na wazazi wa wanafunzi watuhumiwa wakilimbikiziwa jukumu la kugharimia mali yaliyoteketea. Je, mbona visa hivi vya utovu wa nidhamu vikaongezeka maradufu? Mbona zamani visa kama hivi havikuwapo kwa kiwango kikubwa? je, shule zetu zimekuwa nyanda mahsusi za kutoa mafunzo ya uhalifu?

Ni bayana kuwa ukosefu wa nidhamu ndicho chanzo kikuu cha kutekeleza maovu. Binadamu akosaye uadilifu hutenda unyama ushindao wanyama waliojaaliwa akili ndogo. Imebainika kuwa katika shule nyingi za wavulana, tabia chakaramu ya ufiraji huendelea. Wasimamizi wa shule husika, ijapokuwa wanaweza kuujua ukweli, aghalabu watajaribu kulikinga jua kwa ungo kama sika vitanga vyao.

Je, nani akavijongeza vyanda motoni na kukosa kuchomeka? Matumizi ya dawa za kulevya miongoni mwa wanafunzi hawa ni jambo la kawaida. Si ajabu baada ya uchunguzi wa polisi, wanapata wanafunzi waliokuwa katika mstari wa mbele kuteketeza shule ni waraibu wa mihadarati.

PIA SOMA: Mahakama yampiga marufuku mmiliki wa Solai kusafiri nje ya nchi

Shule za wasichana hazisazwi katika uozo huu wa jamii. Visa vya hivi juzi katika shule moja hapa Nairobi vilidhihirisha dhahiri shahiri kuwa tabia chakaramu ya usagaji ilikuwa ikiendelea miongoni mwa wanafunzi hao! Msalie Mtume! Ulimwengu umekwishapasuka. Siku hizi si kama zamani. Wasichana wengi hutumia dawa za kulevya na kuwa kero shuleni hususan kwa wanafunzi wale wengine. Uchunguzi zaidi ulibainisha kuwas baadhi ya wanafunzi hawa mahulukutabu shuleni ni watoto wa watu wenye ushawishi mkubwa serikalini. Jambo hili huwafanya walimu kuchelea kuwaadhibu wakiogopa matokeo ya hatua zao.

Hebu fikiria wewe mzazi, utahisije mwanao akijiunga na shule ya upili halafu katika mwaka wake wa pili anabadilika tabia na kuwa sugu? Mwana aliyeonesha nia kuwa ya kusoma akibadilika na kuanza kuvuta sigara, kunywa pombe, kuvuta bangi na kuhusishwa na visa vya ubakaji! Wazazi wengi nchini wametelekeza wajibu wao. Wakenya tuamke kumekucha na tuelewe kinachoendelea kuwarusha wana wetu katika lindi la uozo.

Ni malezi mabovu. Mzazi aelewe kuwa kulipia mwana karo shuleni asome sio mwisho wa malezi. Kujigamba mbele ya walimu ati wewe unafanya kazi nje ya nchi na kutuma karo yote ya mwaka mara moja…ilhali kupatikana kwako nyumbani ni nadra, hilo silo suluhu. Siku hizi mwalimu ametwika majukumu mengi. Yeye ndiye mwalimu darasani. Yeye ndiye mlezi wa mtoto. Yeye ndiye mtoa ushauri nasaha kwa mtoto atokaye nyumbani akiwa na matatizo ya kisaikolojia eti wazazi walivurugana.

PIA SOMA: Raia Mkenya awasili Zimbabwe kwa kesi ya kuupinga ushindi wa Mnangagwa

Jukumu kuu la mzazi ni malezi na kumfunza mtoto maadili. Jukumu la mwalimu ni kufunza na niseme kumpiga mwanafunzi msasa kwa kumuongezea hekima na busara. Kupata shahada za uzamili na kwamba wewe ni daktari au rubani na umeshindwa kumfunza mwanao maadili ni mojawapo ya ajabu tunazoshuhudia katika ulimwengu wa leo.

Asilimia kubwa ya wazazi hawajua kuwalea wanao  kwa njia zifaazo. Wahenga walisema kazi za kuzaa kazi ni malezi. Mbona wewe mzazi msomi unakosana na mkeo na kurushiana cheche za matusi mbele ya wanao? Mbona wewe mzazi ukiwa na akili zako timamu unamsuta mwalimu hadharani mbele ya wanao, tena mwalimu huyo ndiye unayetarajia awafune wanao?

Tunafaa kuelewa kuwa lawama kwa sasa hazifai. Ukiwaona vijana wakichoma shule, walishuhudia mwanasiasa akiwachochea wananchi kuchoma majengo fulani.Tusipochukua hatua, basi majuto ni kwetu maana mchelea mwana kulia, hulia mwenyewe.

Leave a comment

Your email address will not be published.