Timu za Nairobi na Bungoma zanusia robo fainali

Nairobi na BungomaBungoma walisalia kileleni katika kundi lao la D baada ya kucheza mechi mbili kwenye uga wa KCB hapo jana.

Timu ya soka ya  jimbo la Nairobi na ile ya Bungoma ziko kwenye nafasi bora ya kufuzu kwa timu 16 bora katika kinyang’anyiro cha mashirikisho ya majimbo kinachoendelea jijini Nairobi baada ya kuibuka washindi katika mechi mbili za mwanzo.

Timu ya Nairobi, ambayo iliichabanga Elgeyo-Marakwet mabao saba kwa sifuri katika mechi yao ya ufunguzi mnamo Jumatatu, haikupata upinzani wowote mwingine baada ya kikosi cha jimbo la Wajir kukosa kufika.

Mechi nyingine iliyoratibiwa kuchezwa baina ya Nairobi na Migori ilikosa kuendelea baada ya wenyeji kutoafikiana na Migori kuhusu wachezaji wawili. Kesi hiyo ilitarajiwa kuamuliwa jana jioni.

Bungoma walisalia kileleni katika kundi lao la D baada ya kucheza mechi mbili kwenye uga wa KCB hapo jana.

Mwakilishiwadi wa Bukembe Magharibi  Mhe. Lusenaka, Alfred Makhoka na Dennis Mululu walicheka na wavu kila mmoja huku wakiihakikishia Bungoma ushindi wa mabao 3-1 kabla ya kuiadhibu Kajiado kwa kichapo cha mabao 5-0.

Lusenaka na Makokha waling’aa kwenye mechi ya pili huku Mhe. Elvis Abuka, Mhe. Kawa na Magasi wakifungia timu ya Bungoma. Abuka hakuweza kuificha furaha yake bila kusahau kuwaonya wenzake  dhidi ya wapinzani wao.

“Ulikuwa mchezo mzuri ambao timu yetu imeonesha. Kulingana na jinsi tulivyocheza, nina Imani tutafuzu kwa robo fainali. Wachezaji wetu wako tayari kutwaa ushindi. Tuna matarajio makubwa ya kushinda mechi zilizosalia,” Abuka alisema.