Syombua na wanawe wazikwa huku korti ikisitisha kuachiwa kwa Mumewe

Joyce Syombua na wanawe wawili Shanice Maua na Prince Michael walizikwa Jumamosi katika kijiji cha Kyaithani kaunti ya Kitui.

Familia na jamaa waligubikwa na majonzi na jitimai kwa kuwapoteza wapendwa wao, huku watu kadhaa waliohutubu mazishini wakiomba haki itendeke kwa wapendwa wao.

Meja Peter Mugure ambaye ni mshukuwa mkuu katika kesi hii atasalia korokoroni huko King’ong’o. Hii ni baada wakili Peter Maranyi kuomba azuiliwe kwa wiki moja zaidi.

Maranyi alisema kuwa mshukiwa bado hajafanyiwa uchunguzi wa kiakili ambao ulipangwa kufanyika katika hospitali ya Nanyuki.

Aidha wakili wa mshukiwa wakili Cliff Ombetsa alipinga kuwa haki za kikatiba za mteja wake zilikuwa zinakiukwa.

Hakimu wa mahakama ya juu Jarus Ngaa alisema kuwa hakuna sababu kuu ya kunyima upande wa mashtaka ombi lao.

Hakimu huyo alikubali ombi la kuzuiwa kwa mshtakiwa kwa wiki mbili na kuamuru kuwa meja Mugure afanyiwe uchunguzi wa kiakili katika hospitali ya rufaa ya Nyeri. Tarehe mpya ya kufanya maombi zaidi katika mahakama ni Desemba 17.

Meja Mugure anashtakiwa kwa kumwua mkewe Syombua na wanawe wawili.

Miili ya watatu hao ilipatikana imezikwa katika shimo la kina kifupi katika mtaa wa Thingithu eneo la Nanyuki; wiki tatu baada ya watatu hao kuripotiwa kupotea. Inaaminika kuwa walikuwa wameenda kumtembelea meja Mugure katika makazi yake ya kijeshi Laikipia. Huo ndio ulikiwa wakati wa mwisho Syombua na wanawe walipoonekana kuwa hai.

Uchunguzi wa miili ya Syombua na wanawe ulionyesha kuwa Syombua alifariki kwa kupigwa kichwani na wanawe walinyongwa.

PIA SOMA: Mapenzi ya wapenzi kuuana