Safari ya Bobi Wine yakatizwa ghafla

Bobi WineMaandamano yalizuka katika jiji la Kampala mnamo Ijumaaa asubuhi baada ya polisi kumzuilia Mbunge Bobi Wine kwenye uwanja wa kimataifa wa ndege alipokuwa akijiandaa kwenda nje ya nchi kupokea matibabu.

Maandamano yalizuka katika jiji la Kampala mnamo Ijumaaa asubuhi baada ya polisi kuwazuilia wabunge wawili kwenye uwanja wa kimataifa wa ndege wakati walipokuwa wakijiandaa kwenda nje ya nchi kupokea matibabu.

Wananchi waliandamana katika sehemu mbalimbali za jiji hilo, wakichoma tairi za magari na kukusanya mawe na chochote walichopata cha kuziba barabara. Polisi baadaye walisema maandamano hayo yalidhibitiwa.

Wabunge hao akiwemo Robert Kyagulanyi almaarufu Bobi Wine na mwenzake Francis Zaake, walisema walidhulumiwa na vikosi vya usalama wakiwa kizuizini mwezi wa Agosti, hali iliyosababisha maandamano dhidi ya utawala wa rais Yoweri Museveni.

Rais Museveni amepongezwa na mataifa ya Magharibi kutokana na msimamo wake dhidi ya makundi ya kigaidi kwenye ukanda huu wa Afrika Mashariki, lakini akiwa na umri wa miaka 74, Waganda wengi hawana imani naye hasa asilimia 80 ya wale wenye umri wa chini ya miaka 30.

Wabunge hao walikuwa katika harakati za kusafiri nje ya nchi ili kupokea matibabu kutokana na majeraha waliyopata wakiwa kizuizini, wakati polisi walipowatia nguvuni kwenye uwanja wa ndege. Kyagulanyi alishtakiwa kwa makosa ya uhaini kwa tuhuma kwamba aliongoza kundi lililoupiga mawe msafara wa rais Museveni mwezi Agosti ila mahakama ikapendekeza apate matibabu ya madaktari wa kibinafsi baada ya kukaguliwa afya yake.

Wakili wa Kyagulanyi Robert Amsterdam mnamo wiki iliyopita, aliambia shirika la Reuters kwamba mteja wake asingeweza kusimama baada ya kuumizwa alipokuwa kizuizini. Wakati alipofika mahakamani siku moja baada ya wakili wake kutoa madai hayo, Kyagulanyi hakuweza kutembea bila usaidizi.

Kyagulanyi mwenye umri wa miaka 35 ni mwanamuziki aliyejitosa katika ulimwengu wa siasa baada ya kushinda kiti cha ubunge kupitia uchaguzi mdogo uliofanywa mwaka jana. Kyagulanyi, anayejulikana na wengi kama Bobi Wine, amekuwa mwiba kwa serikali ya rais Museveni ambaye ameiongoza Uganda kwa zaidi ya miaka 30, akiungwa mkono na Waganda wengi kutokana na umaarufu wake katika ulingo wa muziki na vilevile anavyoukashifu utawala wa serikali.

“ Waandamanaji walibamba barabara wakitumia majaa ya taka na kuchoma tairi. Iliwabidi  madereva kutafuta njia mbadala ili kufika katikati ya jiji. Maafisa wa usalama na polisi wa kukabiliana na ghasia waliendelea kusafisha barabara,” Dick Nyule ripota wa idhaa mojawapo nchini humo aliliambia shirika la Reuters.

Msemaji wa polisi Luke Owoyesigyire alisema polisi walikuwa jijini kuhakikisha kwamba hakuna mikutano haramu iliyokuwa ikiendelea. Wabunge hao wawili walikuwa miongoni mwa kundi la wabunge watano ambao walizuiliwa mnamo Agosti 13 kwenye mji wa  Arua ulio Kaskazini Magharibi ya Uganda, na kushutumiwa kwa kuurushia mawe msafara wa kisiasa wa rais Museveni.

PIA SOMA: Jeshi la Uganda laomba samahani baada ya kuwapiga wanahabari kwenye maandamano