Polisi watahadharisha wananchi kuwa waangalifu baada ya mlipuko katikati ya jiji

mlipukoMaafisa wa polisi katika eneo la mkasa wa mlipuko kwenye makutano ya barabara ya Latema na Tom Mboya Januari 26, 2019. [Picha/standard.co.ke]

Polisi wanajitahidi kumtafuta na kumkamata mshukiwa anayedaiwa kuwa mwenye mzigo uliobeba vilipuzi.

Kilichosababisha mlipuko huo hadi sasa hakijajulikana. Hata hivyo, vyombo vya usalama vinaripoti kwamba hilo lilikuwa jaribio la kigaidi.

Kikundi kinachoshughulikia kesi hiyo sasa kimetumia picha na video za kamera za usalama kuchunguza mwendo wa aliyekuwa amebeba mzigo huo  na mmiliki wake.

Waliojeruhiwa ni yule aliyekuwa ameubeba mzigo pamoja na muuzaji wa magazeti.

Mlipuko huo ulitokea Jumamosi saa moja usiku, nje ya jumba la Odeon Cinema, kwenye makutano ya barabara ya Latema na Tom Mboya jijini Nairobi. Polisi wamegundua kuwa kulikuwa na misumari mingi iliyotumika kuunda kilipuzi hicho baada ya kupata swichi iliyotumika kuunda kilipuzi hicho..

Kikosi cha uchunguzi kimedokeza kwamba aliyebeba mzigo huo anaweza kuwa mshukiwa au hata shahidi katika kisa hicho.

Tukio hili lilitokea wiki moja tu baada ya watu watano kuvamia jumba la DusitD2 jijini Nairobi na kuwaua watu zaidi ya thelathini  na kuwajeruhi wengine ishirini na nane.

Ubalozi wa Marekani jijini Nairobi vilevile umewatahadharisha raia wake kuwa waangalifu zaidi.

Mkuu wa polisi Joseph Boinett vilevile amewaomba wananchi kutoa taarifa zozote zitakazosaidia vyombo vya usalama kuimarisha usalama na kukabiliana na uhalifu. Pia ameagiza wahudumu katika maduka, hoteli,makanisa, taasisi za elimu na sehemu zote za umma kufanya uchunguzi wa kina kwa kila anayeingia na kutoka.

Wameagiza pia ripoti kutolewa mara moja iwapo wataona jambo lolote lisilo la kawaida.

PIA SOMA: Matiang’i aikaribisha familia ya aliyekuwa mwanajeshi Josphat Nuru ofisini kwake