Nini baada ya KCSE?

Matokeo ya mtihani wa KCSE yametangazwa, na sherehe zimetanda kila mahali kwa wale waliofuzu. Lakini je, waliopata alama kidogo hatima yao ni gani?

Miaka mingi iliyopita, baadhi ya wanafunzi wamejiua au hata kupotea nyumbani kwao kwa muda bila kupatiana, kutokana na kupata alama ambazo hawakukusudia. Hivi leo wengine wanaposherehekea, ni vyema tuwaangazie wale ambao hawakufaulu kufanya vyema, na ambao mara nyingi hutelekezwa na jamii.

Itakuwa jambo la huzuni iwapo tutaskia mwanafunzi amejitoa uhai baada ya kutopata alama alizotarajia. Kabla ya kujiuliza suluhisho kwa tatizo hili, ni vyema tujiulize basi sababu za wanafunzi kujitoa uhai, kwa sababu ya mtihani ambao mara nyingi haisaidii kuchagua mwelekeo wa maisha wa mja.

Utafiti unaonyesha kuwa:
°Kukataliwa na wazazi na jamii baada ya kupata matokeo duni, huwa fanya wengi kujitoa uhai.
°Dhana potovu kuwa chuo kikuu ni lazima ili mtu afaulu maishani,huwafanya wale waliopata alama duni kuamua kujitoa uhai.
°Kwa miaka mingi,serikali haijawashughulikia wanaopata alama duni, hivi wengi wao kupoteza ari ya kuishi.

Iwapo hizi ndizo sababu zinazosababisha vifo hivi, basi kama nchi tunafaa kuchukua hatua gani ili kuliepuka janga hili?
° Wanafunzi wasiofanikiwa kujiunga na vyuo vikuu kupewa ushauri nasaha na wadau kutoka wizara ya elimu,katika kila kaunti. Hafla hizi ziandaliwe ili kuwapa motisha waliopata alama duni, kuhusu jinsi wanavyoweza kujiendeleza kimaisha.
° Serikali yafaa kuongeza vyuo vikuu na vile vya kiufundi na sanaa, ili kila mwanafunzi aendeleze masomo kulingana na maazimio yao ya kimaisha.
° Serikali kubuni nafasi za ajira hapa nchini na hata katika nchi za nje, ili kuwapa kazi wanaokamilisha masomo yao.
° Mtalaa wa elimu kurekebishwa ili kuhakikisha kuwa kila anayesoma anafaidika.

Nikimalizia, ikumbukwe kuwa elimu ni ufunguo wa maisha, lakini isitumiwe kama mbinu ya kuwabagua waliopita na waliokosa kufikia matarajio yao.