Mkuu wa shambulizi la kigaidi Wajir alikuwa mwalimu wa eneo hilo

Basi lililoshambuliwa katika eneo la Wajir.

Mwalimu mkuu wa shule ya eneo la shambulizi Wajir ambapo watu kumi na mmoja walipoteza maisha alisimamia mashambulizi hayo, polisi sasa wasema.

Polisi wamesema kuwa Mohammed Hussein Hassan, amekimbilia Somalia baada ya vikosi vya polisi kutumwa eneo hilo kusaka magaidi hao.

Polisi wanane wa kitengo cha kulinda mifugo na raia watatu waliuliwa baada ya magaidi hao kutenganisha abiria hamsini na sita wa basi hilo katika vikundi viwili. Wakazi wa eneo hilo wakiachwa.

Ripoti zilizoibuka ni kwamba huenda kuna abiria wa gari hilo walioshirikiana na magaidi kufanya shambulizi hilo. Mwalimu huyo aliongoza kikosi cha magaidi kumi na watano katika shambulizi hilo ambalo limeibua maswali kuhusu usalama wa polisi wanaofanya kazi katika maeneo hayo.

Ripoti zimeibuka kuwa baadhi ya magaidi waliingia kisiri nchini Kenya mwisho wa mwezi Novemba ambapo walipewa makazi na mwalimu huyo. Siku ya Jumapili kamishna wa eneo la Kaskazini mashariki Mohamed Birik alisema washukiwa kumi na mmoja tayari wamekamatwa.

“Tunafikiri kuna washiriki ambao ni wenyeji wa hapa. Sio mara ya kwanza vijana wa eneo hili ambao wameingizwa kwa ugaidi kufanya matendo kama hayo,” alisema.

Kati ya kumi na mmoja hao ni dereva na utingo wa basi hilo.

“Tumechukua hatua dhidi ya familia na watu fulani ambao tunadhani wamekuwa wakiwapa makazi magaidi hao,” Birik alisema.

Aidha imeripotiwa kwamba maisha ya polisi hao yangekuwa salama iwapo wangetumia gari la polisi kwani kulikuwa na mafuta ya kutosha Elraham kuwawezesha kusafiri. ila maafisa hao waliulizwa kuchangisha fedha kununua mafuta ya gari la polisi ila wakakataa na kuamua kuabiri basi.

Siku ya Jumamosi vikosi na vyombo vya usalama vilianza operesheni katika maeneo ya Tarbaj na Katulo.

Katika ujumbe ulisomwa na msemaji wa ikulu Kanze Dena siku ya Jumamosi , Rais Uhuru Kenyatta aliwaonya vikali magaidi hao.

“Hakuna mtu atakayeachwa katika kukomesha vitendo vya ugaidi,” Uhuru alisema.

Licha ya kauli za vyombo vya usalama na afisi husika, mashambulizi kwa wananchi ambao si wenyeji wa maeneo ya kaskazini mashariki ya Kenya yamepoteza maisha ya wengi.

Tayari kundi la kigaidi la Al Shabaab limetoa ujumbe kusema kuwa Lilifanya shambulizi hilo.

Serikali ya Kenya bado haijatoa kauli kuhusu ujumbe huo.

PIA SOMA: Syombua na wanawe wazikwa huku korti ikisitisha kuachiwa kwa Mumewe