Mkufunzi wa West Ham Manuel Pelleggrini apewa mechi mbili kuinusuru kazi yake

Imebainika kwamba mkufunzi wa West Ham kutokea taifa la Chile, Manuel Pelleggrini, amepewa mechi ya Jumamosi Kati ya timu hiyo na Chelsea ugenini na mechi nyingine ya Wolves nyumbani ili kukinusuru kibarua chake.

Hayo yakiendelea klabu hiyo imekuwa ikiwawazia wakufunzi, Eddie Howe, Sean Dyche pamoja na aliyekuwa mkufunzi wa Manchester United na  Everton David Moyes ili kuichukua mikoba yake.

Hii ni baada ya West Ham kuendelea kusuasua na kuandikisha matokeo mabovu katika mechi zao za hivi karibuni na hata kudondoka kutoka katika nafasi ya tano Hadi nafasi ya kumi na Saba.

Timu hiyo haijashinda mechi yoyote katika mechi nane ambazo wameshiriki kwenye michuano yote kwa ujumla nchini Uingereza, na kuongeza shinikizo kwa Pelleggrin.

Huenda kibarua chake kikaota nyasi baada ya kuinoa timu hiyo kwa miezi kumi na minane pekee ikizingatiwa kwamba mechi zijazo ni ngumu sana kupata ushindwe wowote ule. Bodi ya West Ham inahofia kumlipa riba ya Euro milioni 6.5 kwenye mkataba wake wa miaka mitatu alioutia sahihi mwezi mei mwaka Jana.

Pelleggrin pia amejikuta kwenye mgogoro na bodi ya timu hiyo baada ya kumpendelea kipa Roberto Jimenez ambaye hajakuwa katika hali nzuri ya kucheza badala ya Adrian. Kipa chaguo la kwanza wa West Ham ana jeraha litakalomweka nje ya michuano yote hadi Januari.

Katika muda wa siku kumi zilizopita wakufunzi Mauricio Pochettino wa Tottenham na Unai Emery wa Arsenal walipigwa kalamu baada ya timu zao kusajili matokeo mabaya katika ligi kuu ya Uingereza.

Huenda pia mkufunzi wa Everton Marco Silva akafutwa kazi baada ya timu hiyo kuendelea na msururu mbaya wa matokeo, ambapo kwa sasa wanashikilia nafasi ya kumi na sita kwenye jedwali la ligi; wakiwa katika hatari ya kushushwa daraja.

Wasimamizi wa klabu ya Manchester United nao hawana Nia ya kumwachisha kazi Ole Gunnar Solksjaer; wakiendelea kumpa muda kukisuka upya kikosi hicho.

Kusoma habari zetu katika lugha ya Kiingereza bonyeza hapa.