Mapigano ya kikabila yasababisha watu 4,000 kukimbia makazi yao

Zaidi ya watu 4,000 wamekimbia makazi yao kufuatia mapigano ya kikabila ya wiki nzima yanayoendelea katika wilaya ya Fizi mashariki ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC).

Sauti ya Amerika (Voa) ilinukuu taarifa asasi za kiraia kwamba mapigano hayo kati ya makabila ya Wanyamulenge, Wafulero, Wabembe na Banyindu yalipamba moto mwishoni mwa wiki, baada ya kundi la wanamgambo wa Nyamulenge kumshambulia na kumuua mkuu wa kijiji kutoka kabila la Wafulero.

Mkuu wa Wilaya ya Fizi, Aime Mutipula Kawaya amethibitisha habari hiyo, na kusema kwamba maelfu ya wakazi kutoka makabila hayo walikimbilia msituni ambapo hawana huduma yoyote kwa hivi sasa.

Kiongozi moja wa shirika la kiraia katika kijiji cha Minembwe, Rugira Nyagatetera ameiambia Sauti ya Amerika kwamba Jumatatu, kuna vijiji kadhaa vilivyochomwa moto na watu wasiojulikana, na kwamba hadi sasa kuna watu wasiojulikana idadi yao ambao wameuawa katika ghasia hizo.

PIA SOMA: Polisi watahadharisha wananchi kuwa waangalifu baada ya mlipuko katikati ya jiji