Mapenzi ya wapenzi kuuana

Enzi hii tunayoishi imejaa visa vya wapenzi kuuana, kwa sababu nyingi.

Baadhi ya sababu za wapenzi kuuana ni pamoja na udanganyifu katika mahusiano, na sababu nyingine nyingi, ambazo ni za kipuzi tu.

Tutazungumzia mpaka lini kama taifa janga hili, la wapenzi kuuana?

Chukulia kwa mfano hivi majuzi, ambapo mwanafunzi wa kidato cha tatu alimwua mwenzake, kwa shutuma ya kumnyima tendo la ndoa.

Ni shetani gani aliyeingilia kizazi hiki? Ni dhahiri kwamba kuna uozo katika jamii ya hivi sasa, kwani watu wanauana kwa kiwango cha juu sana, kwa sababu za kimapenzi.

Ikumbukwe kwamba sababu za kujihusisha katika mapenzi si kujifaidi na ngono, kama inavyodhaniwa na vijana wengi wa kizazi hiki, bali kusudi yake ni kuzuia upweke baina ya watu. Kwa kiwango kikubwa pia kuendeleza jamii.

Wivu uliopo baina ya wapenzi siku hizi ulitoka wapi? Je, utu ulitutoka binadamu na kuwaendea wanyama, nao unyama kutuingia sisi binadamu?

Nikimalizia, ningependa kuiomba serikali, kupitia kwa waziri wa usalama Daktari Fred Matiangi, na wizara nyingine husika, kuchukua hatua mwafaka, kabla janga hili halijamaliza kizazi chetu chote. Chambilecho wahenga, usipoziba ufa, utajenga ukuta.

Kusoma habari zetu katika lugha ya kiingereza bonyeza hapa.