Mambo yameniendea mrama katika utawala wangu, akiri Rais Kenyatta

Rais Uhuru Kenyatta amekiri ni kweli kuna mambo mengi ambayo yamemwendea upogo kinyume cha alivyotarajia katika utekelezaji wa ahadi alizotoa kwa wananchi wakati wa kampeni za uchaguzi uliopita.

Hata hivyo, Rais Kenyatta amejiondolea lawama kuhusu hali mbaya ya uchumi ambayo imefanya maisha kuwa magumu hasa katika sekta za biashara na kilimo.

Alipozungumza Ijumaa wakati wa mkutano wake na viongozi wa Mlima Kenya katika Ikulu ndogo ya Sagana, Kaunti ya Nyeri, Rais alionekana kuwalaumu mawaziri na wabunge kwa hali hiyo, akisema viongozi husika hawajawahi kumwambia kuhusu changamoto zilizopo.

Ilibainika kuwa katika mkutano huo wa faraghani, baadhi ya viongozi walimwambia Rais Kenyatta kuhusu matatizo yanayokumba wananchi hasa wale wa Mlima Kenya waliompigia kura kwa wingi.

“Ninashukuru viongozi kwa kuleta maswala haya ambayo sote tulichaguliwa kutatua kwa niaba ya wananchi. Hata hivyo, haya mambo yote ambayo yamewasilishwa hapa hayajawahi kufikishwa kwangu. Badala yake, ninachosikia katika runinga, televisheni na mitandao ya kijamii ni matusi na hadithi kuhusu uchaguzi wa 2022. Hawajaniletea sheria wala sera zinazohitajika kubadili hali,” akasema Raia Kenyatta.

Katika sekta ya kibiashara, kumekuwa na malalamishi kwamba utawala wa Jubilee ulibuni sera kali zinazotatiza uwekezaji na ujasiriamali.

Kwa upande mwingine, sekta ya kilimo imeathirika kutokana na sababu mbalimbali ikiwemo bei ya juu ya pembejeo na uagizaji bidhaa za kilimo kwa bei ya chini kutoka nchi za nje kama vile Uganda na China.

Wakulima ambao wametatizika zaidi katika miaka ya hivi majuzi ni wa kahawa, majani chai na miwa, huku wafugaji wa kuku na ng’ombe wa maziwa pia wakilia kuhusu hasara wanazopata.

Ili kusoma habari zetu katika lugha ya Kiingereza bonyeza hapa