Mafuriko yatatuua mpaka lini?

Miezi mitatu sasa, mvua imenyesha kwa wingi hapa nchini, na kusababisha uharibifu wa Mali. Hili lilitokea baada ya muda mrefu wa kiangazi, uliokuwa umekithiri. Lakini je, mbona watu wateseke katika kiangazi na mafuriko? Tumejitayarisha kama nchi kukabiliana na majanga?

Si mara ya kwanza nchi yetu kukumbwa na mafuriko. Ni jambo ambalo limetokea kwa miaka mingi, na si hapa nchini pekee, kwani hata nchi zingine hukumbwa na mafuriko. Mbona katika enzi ya sasa, watu wafe kutokana na athari za mafuriko? Mbona serikali tunazozichagua zisichukue hatua mwafaka kulikabili janga hili?

Jambo linalohuzunisha zaidi ni kuona jinsi nchi zingine za Afrika zilivyojipanga kukabiliana na majanga. Misri kwa mfano, ni nchi iliyo katika jangwa, lakini bado huzalisha mazao ya kulisha nchi nzima. Hii ni kwa sababu ya kujipanga kwao. Kenya kwa mfano, mabwawa yaliyofaa kujengwa yamesimamishwa kutokana na kesi za ufisadi. Tufanye nini ili kukabili majanga yatokanayo na mafuriko?

Jambo muhimu ni kuwasikiliza, na kuwa na imani na halmashauri ya utabiri wa hali ya anga. Kwa miaka mingi, tumekuwa watu wenye kupuuza ushauri wao. Ikumbukwe kuwa kabla ya mvua hizi nyingi, tulipewa onyo lakini kama kawaida, wengi wetu walipuuza. Hivyo basi, itakua bora kwa serikali kuwekeza vilivyo katika halmashauri hii, ili kuwapa uwezo zaidi wa kututabiria hali ya anga kwa usahihi zaidi wakati wote.

Serikali pia yafaa kuhakikisha ujenzi wa mabwawa unaendelezwa. Mabwawa yanayohusishwa na kesi za ufisadi kama zile za Arror na Kimwarer, zichunguzwe na kandarasi hiyo ya ujenzi kupewa wanakandarasi wengine.

Wananchi wanaoishi katika sehemu zinazokumbwa na maporomoko wakati wa mvua kuhama kwa wakati ufaao. Wengi wetu husubiri mpaka wakati ambapo mvua inanyesha ndipo tuhame, na mara nyingi huwa tumechelewa, na kusababisha wengi kupoteza maisha yao.

Mwisho, ni vyema tupande miti. Sababu kuu ya mabadiliko katika hali ya anga duniani,ni ukataji miti bila kupanda nyingine. Tupande miti, ili kuzuia maafa siku za usoni.

PIA SOMA: Ziko wapi ahadi tulizopewa na serikali ya Jubilee?