Jamaa anayefuga simba kwa ajili ya ulinzi wa nyumba yake aamriwa kufika kituo cha polisi

Simba aliyepatikana akilinda nyumba ya makazi siku ya jumatatu.

Mmiliki wa nyumba moja nchini Nigeria, ameamua kumtumia simba kuilinda nyumba yake mjini Lagos.

Simba huyo wa miaka miwili aliripotiwa kuonekana katika nyumba moja ya makazi iliyo karibu na shule na kundi la jopokazi siku ya Ijumaa.

Simba huyo alikamatwa na kuhamishiwa katika hifadhi ya wanyama ya Bogije Omu mjini Lekki, mkuu wa jopo kazi hilo aliiambia BBC.

Mmiliki wa mnyama huyo ameamriwa kufika katika kituo cha polisi mara moja la sivyo akamatwe.

Kundi hilo linalojihusisha na masuala ya usafi wa mazingira na kitengo cha upambana na uhalifu mjini Lagos liliingilia suala hilo baada ya wakazi kuwasilisha ripoti kwa wizara ya mazingira.

Msimamizi wa shule hiyo amesema kuwa walitilia maanani usalama wa watoto.

Inaaminika kuwa simba huyo aliletwa katika nyumba hiyo miezi miwili iliopita.