Harambee Starlets waibamiza Uganda 3-0 katika kipute cha CECAFA

Harambee Starlets imekamilisha mechi zake za Kundi B bila kushindwa mechi yoyote baada ya kuicharza Crested Cranes ya Uganda 3-0 kwenye mashindano ya soka ya wanawake ya Afrika Mashariki na Kati (Cecafa) uwanjani Chamazi jijini Dar es Salaam, Tanzania, Alhamisi.

Starlets ilinyamazisha Uganda kupitia mabao ya Mercy Airo na Mwanahalima Adam Jereko.

Kipa wa Starlets, Annedy Kundu alizima Uganda kurejea mechini alipofanya kazi ya ziada ya kuondosha shuti hatari kutoka kwa Fauzia Najjemba dakika ya 87 kabla ya nguvu-mpya Jentrix Shikangwa kugonga msumari wa mwisho dakika ya 90. Shikangwa aliingia nafasi ya Janet Bundi dakika ya 70.

Kenya imemaliza juu ya kundi lake kwa alama tisa ikifuatiwa na Uganda (sita) nayo Ethiopia imejiondolea aibu ya kubanduliwa nje mapema baada ya Djibouti 8-0.

Starlets italimana na Burundi nayo Uganda ivaane na Tanzania katika mechi za nusu-fainali hapo Novemba 23.

Tanzania pia ilishinda mechi zake zote za Kundi A dhidi ya Sudan Kusini (9-0), Burundi (4-0) na Zanzibar (7-0).

Burundi ilimaliza ya pili katika kundi hilo baada ya kupepeta Zanzibar 5-0 na Sudan Kusini 3-0. Sudan Kusini ilizoa ushindi mmoja iliposhangaza Zanzibar 5-0. Fainali ni Novemba 25.