Droo ya UEFA kuleta Ronaldo Old Traford

UEFAChristiano Ronaldo (kwenye picha) na Paul Pogba droo ya UEFA itawarudisha kuchezea katika uga waliouhama.

Klabu ya Manchester United inayooongozwa na mkufunzi Jose Mourinho imewekwa katika kikundi kimoja kitakachowafanya wachezaji mahiri Paul Pogba na Christiano Ronaldo kurudi kucheza katika nyuga walizozihama. Hii ni baada ya droo ya kiputecha UEFA kufanywa Alhamisi, 30 Agosti jijini Monaco.

Huku presha ikizidi kutanda ugani Old Trafford kutokana na ubutu wa wachezaji wa Man United kutinga mabao, urejeo wa Christiano na kucheza dhidi ya timu yake ya zamani kunapigiwa upatu kuleta msisimko zaidi katika kikosi chote cha timu hiyo. Man United pamoja na Juventus wameratibishwa katika kundi la H pamoja na Valencia ya Uhispania na Young Boys kutoka Uswizi.

Hata hivyo, msisimko unatarajiwa katika kundi la B ambapo mibabe wa soka Barcelona walio na mchezaji mahiri wa Ajentina Lionel Messi, Tottenham yake Mkenya Victor Wanyama, PSV Eindhoven kutoka Uholanzi na Internazionale almaarufu Inter Milan watatafuta nafasi ya kufuzu katika raundi ya timu kumi na sita bora katika kombe lililo na ushabiki mkubwa zaidi baada ya lile la Dunia.

Timu nyingine zilizowakilisha EPL katika mechi ya makundi ni Liverpool katika kundi C, na Manchester City katika kundi F. Liverpool FC anayochezea Mohamed Salah itachuana na Napoli ya Italia, PSG-yake kinda mahiri Kylian Mbappe kutoka Ufaransa na FK Crvena Zvezda almaarufu Red Star Belgrade ya Serbia.

Mabingwa wa ligi ya Uingereza Manchester City wanaojivunia huduma zake Sergio Aguero wana kila sababu za kutabasamu baada ya kuwekwa katika kundi A wakicheza dhidi ya Shaktar Donetsk ya Ukraine, Lyon ya Ufaransa na Hoffenheim ya Ujerumani.

Mabingwa watetezi wa kipute hicho, Real Madrid nao watatifuana mavumbi na wapinzani wao Roma ya Italia, CSKA Moscow ya Urusi na Viktoria Plzen ya Jamhuri ya Chek katika kundi G. Mihemko zaidi inatarajiwa katika kundi D baada ya Lokomotiv Moscow ya Urusi kuwekwa pamoja na Porto ya Ureno, Schalke 04 ya Ujerumani na Galatasary ya Uturuki.

Atletico Madrid kutoka Uhispania nao wana kila hofu katika kundi la A licha ya kusajili mchezaji mahiri wa Ufaransa Thomas Lemar. Hii ni baada ya kuwekwa katika kundi la Dortmund ya Ujerumani inayojivunia ushambulizi wake Mario Gotze, Monaco ya Ufaransa iliyo na straika matata Radamel Falcao na timu ya Brugge yenye tajriba kubwa katika michuano hii kutoka Ubelgiji.

Msimu huu huenda ukawa wake Adjen Robben kuonyesha ubabe wake huku akipania kustaafu mwishoni mwa mwaka ujao. Timu yake ya Bayern Munich imewekwa katika kundi la E kuchaniana sare na Benfica ya Ureno, Ajax ya Uholanzi na AEK Athens ya Ugiriki.

Mechi hizo zitang’oa nanga kuanzia tarehe 18 Septemba mpaka tarehe 12 Desemba. Raundi ya maondoano ya timu kumi na sita itaanza tarehe 12 Februari, 2019 huku fainali ikipaniwa kuchezwa katika uwanja wa Estadio Metropolitano inayomilikiwa na Atletico Madrid, jijini Madrid katika taifa la Uhispania.

PIA SOMA: Mourinho mwishowe azungumza baada ya United kushindwa Shire Kuli na Brighton