Dadake Jacque, Cathylene Maribe amliwaza kwa masaibu anayopitia

Cathylene MaribeCathylene Maribe (kushoto) na dada yake Jacque Maribe.

Familia ya Jacque Maribe inazidi kumpa matumaini wakati huu wa kipindi kigumu.

Dada yake Cathylene Maribe na baba yake Mwangi Maribe wamekuwa naye tangu alipokamatwa na kufikishwa kortini huku wakimpa nguvu na ustahimilivu kwa yale yanayomkabili.

Masaibu ya Jacque yalianza mwezi wa Septemba tarehe 27 wakati alipohitajika kufika kwenye kituo cha polisi cha Kilimani ili kuandikisha taarifa kuhusiana na mauaji ya Monika Kimani.

Jacque aliandamana na baba yake kwenda kituo cha polisi, huku Wakenya wakishangazwa na jinsi baba yake alivyomzuia bintiye dhidi ya wanahabari waliokazana kumpiga picha.

Jacque na mpenzi wake Joseph Irungu walifikishwa katika mahakama ya Milimani mnamo Jumanne Oktoba tarehe 9. Wawili hao walihusishwa na kesi ya mauaji baada ya mkurugenzi wa kesi za jinai kupitia ripoti ya uchunguzi.

Mwanahabari huyo alitiririkwa na machozi pindi alipofikishwa kortini. Cathylene Maribe dada yake Jacque alimtumia ujumbe wa kumliwaza siku moja baada ya kutoka kortini.

“Uchungu ninaohisi moyoni mwangu hauna kifani…Lakini nina utulivu rohoni kwa sababu najua ni Mungu anatutumia kudhihirisha kwamba yeye ndiye Yehovah…” aliandika Cathylene.