Athari ya ufisadi kwa taifa

Historia ya baa la ufisadi nchini ni la tangu enzi za istiimari wakati Kenya ilikuwa chini ya utawala wa kaburu. (Picha/hisani)

Ufisadi ni janga hatari duniani. Nchi yoyote ile inayokumbwa na janga hili na kukosa kuwajibika kukabiliana nalo vilivyo, hatimaye hulemaa kiuchumi. Kutokana na ufisadi, utajiri wa nchi huwa mikononi mwa wachache walalahai huku mamilioni ya wananchi walalahoi wakiteseka.

Historia ya baa la ufisadi nchini ni la tangu enzi za istiimari wakati Kenya ilikuwa chini ya utawala wa kaburu. Rais wa kwanza wa nchi Mzee Jomo Kenyatta hakuwajibika ilivyopaswa kuliangamiza zimwi la ufisadi lingali changa. Huo ndio wakati, wananchi wachache walipoichukua fursa hiyo na kujinyakulia mashamba maddar bassar. Huo ndio wakati mbegu ya ufisadi ilipopandwa, ikapaliliwa na kustawi.

Katika awamu za rais Moi na Mwai Kibaki, zimwi la ufisadi lilikwishapata nguvu na makali ya kutisha. Sakata za wizi wa mabilioni ya fedha hazijaanza kutajwa hapa nchini jana wala juzi. Jambo la kutamausha walilofanya marais hao baada ya vyombo vya habari kuvuvumua habari hizo ni kutangaza kuundwa kwa tume za uchunguzi. Ni tume zilizoundwa na hata hivi sasa zinaundwa ili kuwafumba macho wananchi. Ni tume zisizozalisha matunda hata!

Tangu awamu ya rais Uhuru Kenyatta, wizara mbali mbali zimehusishwa na kashfa za ufisadi. Mabilioni ya fedha yamepotea. Hivi karibuni misururu ya visa vya ufisadi na ubadhirifu wa mali ya umma vimeshuhudiwa. Je wahusika wamefanyiwa nini? Kenya imegeuka kuwa jukwaa la maigizo ya ufisadi! Onyesho hili likitokea na kushuhudiwa, lapisha jingine la ajabu zaidi na visa vya kuifisidi nchi vyawa jambo la kawaida.

Utovu wa nidhamu miongoni mwa watumishi wa serikali umebainika bayana. Baadhi yao wakiwa mawaziri, watu wanaotarajiwa kutoa kielelezo bora kwa wananchi wamenukuliwa wakitema kauli mbovu zilizopungukiwa na hekima. Serikali nayo imelegeza makali yake. Leo vyombo vya habari vinatangaza kwamba kigogo fulani katiwa mbaroni. Siku mbili tatu habari zinapasua anga kuwa kaachiliwa kwa dhamana. Ilivyo kawaida na desturi hapa nchini kwa miaka mingi, wenye uwezo wa kifedha huwa na ushawishi mkubwa mno kwa serikali. Kwa hivyo inakuwa vigumu kusikia kigogo huyo alifungwa gerezani.

Mafisadi hawana aibu. Wasemao husema wenye haya wana mji wao. Hawa wetu wanaoipora serikali wasiibakishe kitu, bado wana umero wa kutaka wateuliwe katika nyadhifa mbalimbali za uongozi. Je, kiongozi aliyehusishwa na ufisadi na bado ana kesi tumbi mahakamani kuhusiana na tuhuma hizo anafaa kuwania wadhifa wowote? Jibu ni la ila hapa Kenya mambo ni mfarka kabisa. Wale wenye kesi zilizorundikana kortini au wengine wameshahusishwa na visa vya uvunjaji wa sheria ndio wanaochaguliwa! Ukistaajabu ya chawa utayaona ya kunguni.

Vita dhidi ya ufisadi vinaanza na sisi wananchi. Mjeledi wa kiongozi fisadi ambaye amezoea vya kunyonga na vya kuchinja haviwezi upo kwenye namna ya upigaji kura. Hatufai hata kidogo kumpigia kura  kiongozi ambaye ameshawahi kutajwa katika kashfa za ufisadi. Jamani tukalifuata hili, ni viongozi wachache hapa nchini wangesalia madarakani.

Inasikitisha kuona kuwa mwizi aliyeiba kuku wa shilingi mia tano kule kijijini akifikishwa mahakamani na kuhukumiwa kifungo mara moja ilhali mtuhumiwa wa wizi wa milioni mia moja, anakamatwa na kuachiliwa kwa dhamana. Baada ya mwaka mmoja au miwili, faili ya kesi yawa haionekani na kesi hiyo inatupiliwa mbali. Je, huu ndio uongozi ufaao? Simtetei maskini aibaye kuku lakini wote wawili ni wezi na isemwavyo sheria ni jambeni inafaa kukata mbele na nyuma bila kuegemea kwa mkata asiye na uwezo wa kumchukua wakili amtetee mahakamani.

Kila mwananchi ameshasikia sakata ya sukari yenye madini ambayo majuma kadhaa yaliyopita ilitamalaki katika kila chumba cha habari. Kamati ya bunge iliundwa ili kufanya uchunguzi lakini wapi! Kumbe baadhi ya watuhumiwa ni watu wenye ushawishi mkubwa serikalini. Habari za kuaminika zinaarifu kuwa wengi wa wabunge walizunguka mbuyu na kuhakikisha kuwa hatua zilizotarajiwa kupigwa katika juhudi na jitihada za kuupiga vita ufisadi zililemazwa.

Watu wanaotuhumiwa kuwa mafisadi wanatiwa mbaroni wakiachiwa. Mwisho kesi zao zinatupiliwa mbali eti hakuna ushahidi wa kutosha uliopatikana! Jamani huu ni uozo. Baadhi ya wale wanaotamani kuiongoza nchi hii ifikapo mwaka 2022, wana kesi nyingi za uporaji wa mali ya serikali na hilo ni jambo wazi, paruwanja linalojulikana. Ni jukumu la Wakenya hata mwanasiasa fisadi akijaribu kutumia vipi nyama ya ulimi, asipigiwe kura au tume ya uchaguzi isiidhinishe awanie nafasi yoyote ile. Kwa kufanya hivi, mwananchi atakuwa ameanza kuzinduka na kujua maana ya kupiga kura.

Iwapo rais uhuru Kenyatta anataka kuacha historia ya kukumbukwa kwa lolote zuri, basi achukue hatua zifaazo bila kujali atapata adui wangapi. Mafisadi wakamatwe na kuwekwa kizuizini bila dhamana yoyote. Mali yote iliyofichwa katika mataifa ya ng’ambo ichukuliwe na mwishowe wote hao watiwe magerezani. Hizo ndizo hatua ambazo zitaweza kumtakasa na kumuondolea lawama zozote ufikapo muda wake wa kuondoka madarakani la sivyo, historia itaandikwa chambilecho wazungu: a pen is mightier than a sword yaani kalamu hutema mambo yenye nguvu kuliko upanga uuao.

Shime wananchi tuungane tuuangamize ufisadi. Ukiwa wewe ni Mkenya kindakindaki, tendo la ufisadi lisifanyike machoni pako kisha unyamaze. Nitayatamatisha makala haya kwa ubeti huu:

Ufisadi kubwa janga, hulemaza n’ti nzima,

Uchumi tuliojenga, ukatota na kuzama,

Na ambalo tulilenga, tukakosa kulifuma,

N’ti hubakiya changa, janga tusipolizima.